Hamia kwenye habari

Mahakama Kuu ya Bulgaria iliyo Katika Eneo la Sofia

MEI 20, 2019
BULGARIA

Ushindi wa Mahakama Kuu Wachangia Uhuru wa Ibada wa Mashahidi wa Yehova Nchini Bulgaria

Ushindi wa Mahakama Kuu Wachangia Uhuru wa Ibada wa Mashahidi wa Yehova Nchini Bulgaria

Machi 2019, Mahakama Kuu ya Bulgaria, mahakama ya juu zaidi nchini, ilitangaza maamuzi mazuri katika kesi tatu zilizowahusisha ndugu zetu. Ushindi huo umeweka msingi muhimu wa kisheria kwa ajili ya kulinda uhuru wa ibada wa ndugu zetu nchini pote.

Kesi mbili kati ya hizo zilihusu uchongezi uliofanywa na vyombo vya habari. Katika mwaka wa 2012, gazeti linaloitwa Vseki Den lilichapisha makala yenye habari za uwongo kuhusu imani yetu. Vivyo hivyo, mwaka wa 2014, kituo cha televisheni kinachoitwa SKAT TV kilirusha habari za uwongo kuhusu tengenezo letu. Katika matukio yote mawili, vituo hivyo vya habari vilikataa kukanusha habari hizo vilipoombwa na ndugu zetu. Baada ya kesi kadhaa mahakamani na kukata rufani pia, suala hilo lilifika Mahakama Kuu. Machi 18, 2019, Mahakama Kuu ilitangaza kushindwa kwa kituo cha SKAT TV. Na Machi 26, Mahakama ilitumia uamuzi huo kutoa adhabu kwa gazeti Vseki Den, ilishutumu mwenendo wao na kusema kwamba walitumia “lugha yenye chuki.”

Kesi ya tatu ilihusu unyanyasaji wa kikatili waliotendewa ndugu zetu na kikundi cha kisiasa kinachoitwa VMRO-Bulgarian National Movement. Aprili 17, 2011, ndugu zetu walikutanika ili kuadhimisha kifo cha Yesu. Kiongozi wa kisiasa Georgi Drakaliev wa VMRO alipanga kikundi cha watu 60 wenye hasira kali na kuwashambulia ndugu zetu, wakawaumiza na kuwaacha na majeraha. Ndugu hao waliwasilisha kesi hiyo mahakamani. Na mwishowe kesi hiyo ikafika Mahakama Kuu. Machi 20, 2019, Mahakama ilimhukumu Bw. Drakaliev kuwa na hatia, na kumtoza fidia kwa mambo aliyowatendea ndugu zetu .

Tunashangilia kwa kushinda kesi hizo tatu. Maamuzi haya yaliyofanywa yanaweza kuwa msingi wa kulinda uhuru wa ndugu zetu, na hivyo kuwasaidia “kuishi kwa amani na utulivu na ujitoaji-kimungu kamili.”—1 Timotheo 2:2.