Hamia kwenye habari

Ndugu Shamil Khakimov kabla ya kufungwa gerezani mnamo Februari 2019

MACHI 4, 2021
TAJIKISTAN

Tume ya Uhuru wa Ibada wa Kimataifa ya Marekani Inapanga Kuomba Ndugu Shamil Khakimov Aliyefungwa Tajikistan Aachiliwe Huru

Tume ya Uhuru wa Ibada wa Kimataifa ya Marekani Inapanga Kuomba Ndugu Shamil Khakimov Aliyefungwa Tajikistan Aachiliwe Huru

Nury Turkel, Mkuu wa USCIRF a alitangaza Februari 24, 2021, kwamba atatuma maombi ya kuachiliwa huru kwa Ndugu Shamil Khakimov, mwenye umri wa miaka 70, ikiwa sehemu ya Mradi wa USCIRF wa Wafungwa wa Kidini kwa Sababu ya Dhamiri. Katika tangazo lake, Mkuu wa USCIRF, Turkel alisema hivi: “Tangu 2019, mwanaume huyu mzee anayeugua, amekuwa akiteseka katika mazingira mabaya na katika gereza lenye watu wengi, akiwa amefungwa kwa miaka saba na nusu kwa mashtaka ya uwongo. Kifungo hicho kinaweza kumsababishia kifo mwanamume huyo aliyefungwa isivyo haki kwa sababu ya imani yake akiwa ni Shahidi wa Yehova.”

Ndugu Khakimov, anayeishi peke yake baada ya mke wake kufa, ni miongoni mwa Mashahidi 24 katika eneo la kaskazini mwa Tajikistan waliohojiwa na maofisa wa Idara ya Kudhibiti Uhalifu Mkubwa (DOCC) katika mwezi wa Januari na Februari 2019. DOCC ilimkamata Ndugu Khakimov na kumhoji kuhusu tengenezo letu na jinsi alivyokuwa Shahidi wa Yehova.

Ndugu Khakimov aliwekwa kizuizini kwa saa nane na alinyimwa matibabu aliyohitaji baada ya kufanyiwa upasuaji. Alipatwa pia na shinikizo la damu. Hatimaye polisi walipompeleka nyumbani, walichukua vifaa vyake vya kielektroni, Biblia, na nakala za machapisho ya Biblia, na pasipoti. Kwa kuwa pasipoti yake ilichukuliwa, Ndugu Khakimov alishindwa kupata mafao yake ili aweze kulipia matibabu baada ya kufanyiwa upasuaji.

Februari 28, 2019, hakimu wa Mahakama ya Jiji la Khujand aliamuru kwamba Ndugu Khakimov awekwe mahabusu. Muda wake wa kukaa mahabusu uliongezwa mara tatu. Aliendelea kukaa mahabusu kipindi chote cha upelelezi na kesi.

Septemba 10, 2019, alihukumiwa kifungo cha miaka saba na nusu gerezani. Hata hivyo, Julai 4, 2020, ofisi inayosimamia gereza ilimjulisha Ndugu Khakimov kwamba sheria ya Tajikistan ya kutoa msamaha itatumiwa katika hukumu yake, na atapunguziwa miaka miwili, miezi mitatu, na siku kumi. Ataachiliwa huru Mei 16, 2024.

Tunajua kwamba Yehova ataendelea kuwasaidia ndugu na dada zetu ili waendelee kuvumilia wakiwa na subira na shangwe.—Zaburi 20:2.

a Tume ya Uhuru wa Ibada wa Kimataifa ya Marekani