Hamia kwenye habari

SEPTEMBA 18, 2019
UINGEREZA

Ujenzi wa Ofisi ya Tawi la Uingereza, Mfano wa Utunzaji Mazingira, Wakaribia Kumalizika

Ujenzi wa Ofisi ya Tawi la Uingereza, Mfano wa Utunzaji Mazingira, Wakaribia Kumalizika

Ujenzi wa Ofisi ya Tawi ya Uingereza karibu na jiji la Chelmsford, Essex, unatarajia kumalizika Desemba 2019. Tayari mradi huo unatambulika na wataalamu kuwa ni mojawapo ya maeneo yaliyofufuliwa.

Ndugu zetu waliponunua eneo hili mwaka 2015, kulikuwa na rundo la magari mabovu na takataka nyingi zilizotupwa hapo. Wajitoleaji walichimbua na kukusanya uchafu mwingi, kutia ndani maelfu ya tairi za magari—na mengine hata yalitumika wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Kisha wakachuja udongo uliokuwa umechafuliwa ili kuondoa hata mabaki ya uchafu huo. Chochote kilichoonekana kuwa na manufaa kilirudishwa pamoja na udongo ili kitumike. Zaidi ya ndugu na dada 11,000 walijitolea katika kazi hiyo ya kusafisha eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 34, nao wametumia jumla ya saa milioni nne.

Kushoto: Wajitoleaji waliozoezwa wakiondoa takataka ndogondogo mwaka wa 2015; Kulia: Picha ya karibuni ya bustani maridadi ya maua

Ujenzi huo utakapokamilika utakuwa na bustani za maua ya asili ya eneo hilo na bustani za mimea mingine. Kutakuwa na mabwawa, maua ya porini, pamoja na shamba la miti ya matunda. Lengo si kutokeza eneo lenye kupendeza tu. Litakuwa pia makao ya wanyama pori ambao asili yao ni eneo hilo. Pia, maji yatashughulikiwa kwa njia ya kawaida, miti iliyokuwepo kwa muda mrefu pamoja na vichaka vya asili vitadumishwa. Lengo litakuwa pia kuongeza mimea ya asili ya eneo hilo na kufanya wenyeji wafurahie zaidi mandhari ya ujirani wao.

Ndugu Paul Rogers, wa Halmashauri ya Mradi wa Ujenzi (CPC) alisema hivi: “Eneo tulilonunua lilikuwa limepuuzwa na kutumiwa vibaya kwa miaka mingi. Mabadiliko yalianza na jeshi la wajitoleaji waliochambua takataka zote kwa umakini sana. Hatua hiyo ilifuatiwa na kusawazisha ardhi kwa njia iliyozingatia rasilimali zilizopo kwenye eneo hilo. Vilevile, mamia ya miti, michongoma, na mimea mingine ilioteshwa. Matokeo ya mradi huo wenye kupendeza, yanapatana na maneno yaliyo katika Ezekieli 36:35, 36: ‘Na watu watasema: “Nchi iliyokuwa ukiwa imekuwa kama bustani ya Edeni”. . .  Na mataifa . . .  yatalazimika kujua kwamba mimi mwenyewe, Yehova, nimejenga kilichobomolewa, nami nimepanda kilichofanywa ukiwa.’”

 

Dada wawili wakitoa takataka kwenye bwawa. Matrekta yalitumiwa kutoa takataka kubwa na matope bwawani, kisha takataka ndogondogo pamoja na majani yaliyobaki yakatolewa kwa mkono. Zaidi ya mimea 8,000 ya majini imepandwa, ili kuchangia usafi wa maji hayo

Mojawapo ya mabwawa ambayo ni sehemu ya mfumo wa kusafisha maji, linakusanya maji yanayotoka kwenye barabara iliyo karibu na kutoka kwenye ofisi ya tawi. Upande wa kushoto wa picha ni kituo cha basi kilicho na sehemu ya watu wa eneo hilo kufurahia mandhari ya bustani letu

Kikundi cha ndugu watatu wakipanda mti katika eneo la ujenzi. Karibu miti 15,000, vichaka, na mimea mingine imeoteshwa

Miti sita ya mzeituni, iliyokadiriwa kuwa na miaka 100 hivi, imepandwa mbele ya eneo la mapokezi la jengo la ofisi

Kikundi cha akina dada wakipigwa picha walipokuwa wakiendelea na kazi. Zaidi ya miche 18,000 ya maua imeoteshwa katika maeneo yenye miti mingi. Angalau asilimia 80 ya mimea iliyopandwa ni ya maua ya asili ya eneo hilo

Maua, vichaka, na miti imeoteshwa kwa mpangilio mzuri kwenye bustani inayozunguka kijia cha kuingilia jengo la Makazi F