Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Mbinu ya Nyuki ya Kutua

Mbinu ya Nyuki ya Kutua

NYUKI anaweza kutua salama mahali popote bila tatizo. Anawezaje kufanya hivyo?

Fikiria jambo hili: Ili atue salama, nyuki anahitaji kupunguza mwendo wake kabisa kabla ya kugusa mahali anapotaka kutua. Njia moja rahisi ingekuwa kupima kasi yake na umbali wa kufika pale anapokusudia kutua, kisha apunguze kasi hiyo hatua kwa hatua kulingana na umbali uliobaki. Hata hivyo, njia hiyo ni ngumu kwa wadudu wengi, kwa sababu wana macho ambayo hayawezi kupima umbali.

Macho ya nyuki yanaona kwa njia tofauti sana na ya mwanadamu anayeweza kuona na kukadiria umbali. Inaonekana nyuki hutumia njia rahisi ya kwamba kadiri anavyosogelea kitu, kitu hicho kinazidi kuonekana kikubwa. Kadiri anavyozidi kukikaribia, kinazidi kuongezeka ukubwa kwa kasi zaidi. Uchunguzi uliofanywa na Australian National University unaonyesha kwamba nyuki hupunguza mwendo wake ili kasi ya kuongezeka ukubwa wa kitu anachotazama ibaki vilevile. Anapofika mahali alipokusudia kutua, mwendo wake unakuwa umepungua sana, na hivyo kumwezesha kutua salama.

Jarida la Proceedings of the National Academy of Sciences liliripoti hivi: “Mbinu hii rahisi ya kutua . . . itafaa sana ikiwa itatumiwa katika mfumo wa kuongoza roboti zinazoruka angani.”

Una maoni gani? Je, mbinu ya nyuki ya kutua ilijitokeza yenyewe? Au ilibuniwa?