Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi ya Kudhibiti Matumizi ya Kileo

Jinsi ya Kudhibiti Matumizi ya Kileo

 Watu fulani huhisi kwamba wanahitaji kunywa kileo zaidi wanapokuwa na mkazo, wanapohisi upweke, au wanapohisi kuwa wamechoka kwa sababu hawana lolote la kufanya. Je, siku hizi unakunywa kiasi kikubwa kuliko hapo awali? Ikiwa ndivyo, unaweza kufanya nini ili kuhakikisha kwamba hunywi kupita kiasi au kwamba wewe si mraibu wa kileo? Fikiria habari hii inayofaa inayoweza kukusaidia kudhibiti matumizi ya kileo.

 Kunywa kwa kiasi kunamaanisha nini?

 Biblia inasema nini?: “Usiwe miongoni mwa watu wanaokunywa divai nyingi mno.”—Methali 23:20.

 Fikiria hili: Biblia haishutumu kunywa kileo kwa kiasi. (Mhubiri 9:7) Hata hivyo, inatofautisha kati ya kunywa kwa kiasi, kunywa kupita kiasi, na ulevi. (Luka 21:34; Waefeso 5:18; Tito 2:3) Hata ikiwa mtu hatalewa, kunywa kileo kingi kunaweza kukuongoza ufanye maamuzi mabaya au kudhuru afya na uhusiano wako na wengine.—Methali 23:29, 30.

 Wenye mamlaka wengi huonyesha tofauti kati ya kunywa kileo kwa kiasi na kunywa kupita kiasi kwa kutumia vipimo vya kile ambacho mtu anakunywa kwa siku au kwa siku kadhaa ndani ya juma moja. a Hata hivyo, kileo huwaathiri watu kwa njia tofauti, na kuna nyakati ambapo uamuzi bora ni kuamua kuepuka kunywa kabisa. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni:

 Hata chupa moja au mbili zinaweza kuwa nyingi kupita kiasi—ikiwa:

  •   Unaendesha gari au kutumia mashine.

  •   Wewe ni mjamzito au unanyonyesha.

  •   Unatumia dawa fulani.

  •   Una matatizo fulani ya afya.

  •   Huwezi kudhibiti kunywa kileo.

 Jinsi ya kujua ikiwa unatumia kileo vibaya

 Biblia inasema nini?: “Acheni tuzikague na kuzichunguza kwa makini njia zetu.”—Maombolezo 3:40.

 Fikiria hili: Unaweza kujilinda dhidi ya madhara yanayosababishwa na kileo ukichunguza kwa ukawaida mazoea yako ya kunywa na kuyabadili, ikiwa kuna uhitaji wa kufanya hivyo. Angalia ikiwa mambo yafuatayo yanaonyesha umeanza kutumia kileo vibaya.

  •   Unategemea kileo ili uwe na furaha. Unahisi kwamba lazima unywe ili utulie, uchangamane na marafiki, au ili ujifurahishe. Unakunywa ili kukabiliana na matatizo yako.

  •   Unakunywa zaidi ya ulivyokuwa ukinywa awali. Unakunywa mara nyingi zaidi. Unachokunywa kina wastani wa juu zaidi wa kileo, na ili uhisi umeridhika unahitaji kunywa kiasi kingi zaidi kuliko ulivyozoea.

  •   Mazoea yako ya kunywa yamesababisha matatizo nyumbani au kazini. Kwa mfano, pesa nyingi zaidi zinatumiwa kununua kileo badala ya kushughulikia mahitaji ya lazima.

  •   Unafanya maamuzi hatari baada ya kunywa, kama vile kuchagua kuendesha gari, kuogelea, au kuendesha mashine.

  •   Wengine wana wasiwasi kuhusu mazoea yako ya kunywa. Wanapofanya hivyo, unakasirika au kujitetea. Unajaribu kuwaficha wengine mazoea yako ya kunywa, au unasema uwongo kuhusu kiasi ambacho wewe hunywa.

  •   Unapata matatizo kuacha kunywa. Umejaribu kunywa kiasi kidogo zaidi au kuacha kunywa, lakini unashindwa.

 Mambo matano yatakayokusaidia kudhibiti matumizi ya kileo

 1. Panga mikakati.

 Biblia inasema nini?: “Mipango ya wenye bidii hakika huleta mafanikio.”—Methali 21:5.

 Jaribu kufanya hivi: Chagua ni siku zipi katika juma ambazo utakunywa. Jiwekee kiwango utakachokunywa kwa kiasi katika siku hizo. Panga kwamba baada ya kunywa, siku mbili zitapita kabla ya kunywa tena katika juma hilo.

 “Kupumzika kwa ukawaida kwa muda fulani bila kunywa kileo ndiyo njia bora zaidi ya kupunguza uwezekano wa kukitegemea,” linasema shirika la Uingereza linalotoa elimu kuhusu kileo.

 2. Tekeleza mpango wako.

 Biblia inasema nini?: “Malizeni . . . kile mlichoanza kufanya.”—2 Wakorintho 8:11.

 Jaribu kufanya hivi: Jifunze kipimo kinachofaa ni kipi ili uweze kupima na kuhesabu kiasi unachokunywa kwa usahihi. Tafuta vinywaji visivyo na kileo vilivyo na afya unavyoweza kufurahia, kisha uviweke karibu.

 “Mabadiliko madogo yanaweza kupunguza sana uwezekano wako wa kuwa na matatizo yanayohusiana na kunywa kileo,” inasema Taasisi ya Marekani Inayoshughulikia Matumizi Mabaya ya Kileo na Uraibu.

 3. Shikamana na maamuzi yako.

 Biblia inasema nini?: “Acheni ‘Ndiyo’ yenu iwe ndiyo, na ‘Siyo’ yenu, siyo.”—Yakobo 5:12.

 Jaribu kufanya hivi: Uwe tayari kukataa kwa upole lakini kwa usadikisho mtu anapokupa kileo siku inayoingiliana na mpango wako.

 “Ukikataa upesi unapopewa kileo, haitakuwa rahisi kushindwa,” inasema Taasisi ya Marekani Inayoshughulikia Matumizi Mabaya ya Kileo na Uraibu.

 4. Kazia fikira manufaa ya uamuzi wako.

 Biblia inasema nini?: “Ni afadhali mwisho wa jambo kuliko mwanzo wake.”—Mhubiri 7:8.

 Jaribu kufanya hivi: Andika orodha ya sababu zinazokufanya utake kudhibiti matumizi yako ya kileo. Tia ndani mambo kama vile mazoea mazuri ya kulala, kuboresha afya, uchumi, na mahusiano. Unapozungumza na wengine kuhusu maamuzi yako, kazia fikira manufaa badala ya changamoto.

 5. Mtegemee Mungu ili akutegemeze.

 Biblia inasema nini?: “Kwa mambo yote nina nguvu kupitia yule anayenipa nguvu.”—Wafilipi 4:13.

 Jaribu kufanya hivi: Ikiwa una wasiwasi kuhusu mazoea yako ya kunywa kileo, sali kwa Mungu umwombe msaada. Mwombe akupe nguvu na uwezo wa kujidhibiti. b Tenga wakati wa kujipatia hekima inayotumika iliyo katika Neno lake, Biblia. Akiwa upande wako, unaweza kudhibiti matumizi yako ya kileo.

a Kwa mfano, Kituo cha Matatizo ya Uraibu cha Ujerumani kinasema hivi: “Kiasi cha juu zaidi ambacho mtu mwenye afya anaweza kunywa kileo bila kujisababishia madhara . . . kwa wanaume ni gramu 24 za kileo kwa siku na gramu 12 kwa siku kwa wanawake. Kipimo hicho kinalingana lita 0.5-0.6 za bia au 0.25-0.3 za divai iliyo na kileo cha wastani; wanawake wanapaswa kutumia nusu ya vipimo hivyo.”

b Ikiwa huwezi kudhibiti matumizi yako ya kileo, huenda pia ukahitaji kutafuta msaada kutoka kwa wataalamu.