Hamia kwenye habari

Wanawake Katika Biblia—Tunaweza Kujifunza Nini Kutoka Kwao?

Wanawake Katika Biblia—Tunaweza Kujifunza Nini Kutoka Kwao?

Jibu la Biblia

 Katika Biblia, tunasoma kuhusu wanawake wengi ambao maisha yao yanatufundisha masomo yenye thamani. (Waroma 15:4; 2 Timotheo 3:16, 17) Makala hii inazungumzia kwa ufupi tu baadhi ya wanawake wanaotajwa katika Biblia. Wengi wao ni mifano mizuri ya kuiga. Wengine ni mifano ya kuonya.—1 Wakorintho 10:11; Waebrania 6:12.

  Abigaili

 Abigaili alikuwa nani? Alikuwa mke wa mwanamume mkatili aliyeitwa Nabali. Hata hivyo, Abigaili alikuwa mwenye busara na mnyenyekevu, na pia alikuwa mrembo kimwili na kiroho.—1 Samweli 25:3.

 Alifanya nini? Abigaili alitenda kwa hekima na busara ili kuzuia msiba. Yeye na Nabali waliishi katika eneo ambalo Daudi, mfalme mtarajiwa wa Israeli, alikuwa akijificha. Daudi na wanaume wake walipokuwa huko, walilinda makundi ya kondoo ya Nabali yasiibiwe. Lakini Daudi alipowatuma wajumbe kumwomba Nabali chakula, Nabali aliwatukana na kukataa. Daudi alikasirika sana. Kwa hiyo, yeye na wanaume wake wakapanga kwenda kumuua Nabali na wanaume wote wa nyumba yake.—1 Samweli 25:10-12, 22.

 Abigaili alitenda upesi aliposikia kile ambacho mume wake alikuwa amefanya. Aliwapa watumishi wake chakula wampelekee Daudi na wanaume wake, naye pia akawafuata ili kumwomba Daudi awaonyeshe rehema. (1 Samweli 25:14-19, 24-31) Daudi alipoona zawadi yake, unyenyekevu wake, na aliposikia ushauri wake wenye hekima, alitambua kwamba Mungu alimtumia ili kumzuia asimuue Nabali na wanaume wake. (1 Samweli 25:32, 33) Muda mfupi baada ya hapo, Nabali alikufa, naye Abigaili akawa mke wa Daudi.—1 Samweli 25:37-41.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Abigaili? Ingawa alikuwa mrembo na tajiri, Abigaili alikuwa na maoni yenye usawaziko kujihusu. Ili kudumisha amani, alikuwa tayari kuomba msamaha kwa jambo ambalo halikuwa kosa lake. Alishughulikia hali yenye kutisha kwa utulivu, busara, ujasiri, na alitumia nguvu zake za kufikiri.

  •  Ili kupata habari zaidi kumhusu Abigaili, ona makala yenye kichwa, “Alitenda kwa Busara.”

  Debora

 Debora alikuwa nani? Alikuwa nabii wa kike aliyetumiwa na Mungu wa Israeli, Yehova, kuwajulisha watu wake mambo aliyotaka wafanye. Pia, Mungu alimtumia kusuluhisha matatizo yaliyokuwa yakiendelea miongoni mwa Waisraeli.—Waamuzi 4:4, 5.

 Alifanya nini? Nabii huyo wa kike Debora aliwategemeza waabudu wa Mungu kwa ujasiri. Kwa mwongozo wa Mungu, alimwamuru Baraka aliongoze jeshi la Waisraeli likapigane na Wakanaani waliokuwa wakiwakandamiza. (Waamuzi 4:6, 7) Baraka alipomwomba Debora aende naye, alikubali kwa hiari bila woga, naye akatenda kulingana na ombi lake.—Waamuzi 4:8, 9.

 Baada ya kupewa ushindi mkubwa na Mungu, Debora alichangia kutunga sehemu ya wimbo ambao waliuimba pamoja na Baraka kuhusu jambo lililotokea. Katika wimbo huo, alitaja sehemu iliyotimizwa na Yaeli, mwanamke jasiri, katika kuwashinda Wakanaani.— Waamuzi, sura 5.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Debora? Debora alikuwa jasiri na mwenye kujidhabihu. Aliwatia moyo watu wafanye kile kilicho sahihi machoni pa Mungu. Walipofanya hivyo, aliwapongeza kwa ukarimu kwa mambo waliyotimiza.

  Delila

 Delila alikuwa nani? Alikuwa mwanamke aliyependwa na Samsoni, mwamuzi wa Israeli.—Waamuzi 16:4, 5.

 Alifanya nini? Alikubali pesa kutoka kwa wakuu wa Wafilisti ili kumsaliti Samsoni, aliyetumiwa na Mungu kuwaokoa Waisraeli kutoka kwa Wafilisti. Wafilisti walishindwa kumdhibiti kwa sababu alikuwa na nguvu za kimuujiza. (Waamuzi 13:5) Hivyo, wakuu hao walitafuta msaada kutoka kwa Delila.

 Wafilisti walimhonga Delila ili wapate kujua Samsoni alivyopata nguvu zake. Delila alikubali pesa hizo, na baada ya kujaribu mara kadhaa, alifanikiwa kupata siri ya Samsoni. (Waamuzi 16:15-17) Aliwafunulia Wafilisti siri hiyo, nao wakamkamata Samsoni na kumfunga gerezani.—Waamuzi 16:18-21.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Delila? Delila ni mfano wa kuonya. Kwa kuwa alikuwa na pupa, alitenda kwa udanganyifu, alikosa ushikamanifu, na alikuwa mbinafsi akitanguliza masilahi yake badala ya kumtanguliza mtumishi wa Yehova Mungu.

  Esta

 Esta alikuwa nani? Alikuwa Myahudi aliyechaguliwa na Mfalme Ahasuero wa Milki ya Uajemi awe malkia wake.

 Alifanya nini? Malkia Esta alitumia uwezo wake kuepusha kuangamizwa kwa jamii yake. Aligundua kwamba agizo rasmi lilitolewa na Mfalme kuhusu siku ambayo Wayahudi wote waliokuwa wakiishi katika milki ya Uajemi wangeuawa. Njama hiyo ya kikatili ilipangwa na Hamani, aliyekuwa waziri mkuu. (Esta 3:13-15; 4:1, 5) Kwa msaada wa binamu yake, Mordekai, aliyekuwa amemzidi umri, Esta alihatarisha maisha yake kwa kufunua njama hiyo kwa mume wake, Mfalme Ahasuero. (Esta 4:10-16; 7:1-10) Ahasuero aliwaruhusu Esta na Mordekai watoe agizo lingine rasmi lililowaruhusu Wayahudi kulinda uhai wao. Wayahudi waliwashinda kabisa maadui wao.—Esta 8:5-11; 9:16, 17.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Esta? Malkia Esta aliweka mfano mzuri sana wa ujasiri, unyenyekevu, na kiasi. (Zaburi 31:24; Wafilipi 2:3) Licha ya urembo wake na mamlaka aliyokuwa nayo, alitafuta ushauri na msaada. Alipozungumza na mume wake, alitenda kwa busara na heshima, lakini kwa ujasiri. Na katika pindi ambayo maisha ya Wayahudi wote yalikuwa hatarini, alijitambulisha kwa ujasiri kuwa mmoja wao.

  Hawa

 Hawa alikuwa nani? Alikuwa mwanamke wa kwanza kabisa na mwanamke wa kwanza kutajwa kwenye Biblia.

 Alifanya nini? Hawa alikataa kutii amri ya Mungu iliyokuwa wazi kabisa. Hawa aliumbwa akiwa mkamilifu kama Adamu, mume wake, na alikuwa na uhuru wa kuchagua na uwezo wa kusitawisha sifa kama za Mungu, yaani, upendo na hekima. (Mwanzo 1:27) Hawa alijua kuwa Mungu alimwambia Adamu kwamba ikiwa wangekula matunda ya mti fulani, wangekufa. Hata hivyo, alidanganywa na kuamini kwamba hangekufa. Hata aliamini kwamba angekuwa na maisha mazuri ikiwa angeamua kutomtii Mungu. Kwa hiyo, alikula lile tunda na baadaye akamshawishi mume wake ale pia.—Mwanzo 3:1-6; 1 Timotheo 2:14.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Hawa? Hawa ni mfano wa kuonya kuhusu hatari ya kuendelea kukazia fikira tamaa mbaya. Alisitawisha tamaa yenye nguvu sana ya kuchukua kitu ambacho hakikuwa chake, jambo lililopinga amri ya Mungu iliyokuwa wazi kabisa.—Mwanzo 3:6; 1  Yohana 2:16.

  Hana

 Hana alikuwa nani? Alikuwa mke wa Elkana na mama ya Samweli, aliyekuja kuwa nabii maarufu katika taifa la kale la Israeli.—1 Samweli 1:1, 2, 4-7.

 Alifanya nini? Kwa kuwa Hana hakuwa na watoto, alimwomba Yehova faraja. Mume wa Hana alikuwa na wake wawili. Mke huyo mwingine, Penina, alikuwa na watoto; lakini Hana hakuwa na watoto kwa muda mrefu baada ya ndoa yake. Penina alimdhihaki kikatili, lakini Hana alimwomba Mungu faraja. Aliweka nadhiri kwa Mungu, akisema kwamba ikiwa Mungu angempa mtoto wa kiume, angemtoa mtoto huyo atumikie katika hema la ibada lililotumiwa na Waisraeli.—1 Samweli 1:11.

 Mungu alijibu sala ya Hana kwa kumpa Samweli. Hana alitimiza ahadi yake na akamkabidhi mtoto wake mdogo atumikie kwenye hema la ibada. (1 Samweli 1:27, 28) Kila mwaka, alimshonea joho dogo lisilo na mikono na kumletea. Baada ya muda, Mungu alimbariki Hana na watoto watano zaidi—wana watatu na mabinti wawili.—1 Samweli 2:18-21.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Hana? Hana alivumilia majaribu kwa kutoa sala za kutoka moyoni. Sala yake ya shukrani inayopatikana kwenye 1 Samweli 2:1-10 inaonyesha imani yake yenye kina kwa Mungu.

  Yaeli

 Yaeli alikuwa nani? Alikuwa mke wa Heberi, Mwanamume ambaye hakuwa Mwisraeli. Yaeli aliwaunga mkono watu wa Mungu bila woga.

 Alifanya nini? Yaeli alichukua hatua mara moja dhidi ya Sisera, mkuu wa jeshi la Kanaani, alipofika kambini kwao. Baada ya kushindwa na Waisraeli, Sisera alikuwa akitafuta mahali pa kujificha. Yaeli alimkaribisha kwenye hema lake ili ajifiche na apate kupumzika. Lakini alipokuwa akilala, Yaeli alimwua.—Waamuzi 4:17-21.

 Tendo la Yaeli lilitimiza unabii aliotoa Debora: “Yehova atamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.” (Waamuzi 4:9) Na kwa tendo hilo, Yaeli alisifiwa kuwa “amebarikiwa kuliko wanawake wote.”— Waamuzi 5:24.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Yaeli? Yaeli alichukua hatua na kutenda kwa ujasiri. Simulizi lake linaonyesha jinsi Mungu anavyoweza kuelekeza matukio ili kutimiza unabii.

  Yezebeli

 Yezebeli alikuwa nani? Alikuwa mke wa Mfalme wa Israeli, Ahabu. Hakuwa Mwisraeli na hakumwabudu Yehova. Badala yake, alimwabudu mungu wa Wakanaani aliyeitwa Baali.

 Alifanya nini? Malkia Yezebeli alitawala kwa ukatili na kwa mabavu. Alichochea watu wamwabudu Baali na kuchochea uasherati uliokuwa sehemu ya ibada hiyo. Na kwa wakati huohuo, alijaribu kukomesha ibada ya Mungu wa kweli, Yehova.—1 Wafalme 18:4, 13; 19:1-3.

 Yezebeli alisema uwongo na kuua watu ili apate kile alichotaka. (1 Wafalme 21:8-16) Mwishowe mambo ambayo Mungu alitabiri kumhusu yalitimia, alikufa kifo cha kikatili na hakuzikwa.—1 Wafalme 21:23; 2 Wafalme 9:10, 32-37.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Yezebeli? Yezebeli ni mfano wa kuonya. Alikuwa na maadili mapotovu na alikuwa mwenye hila hivi kwamba jina alilopewa linamaanisha mtu asiye na haya, mwenye maadili mapotovu, na asiyejizuia.

  Lea

 Lea alikuwa nani? Alikuwa mke wa kwanza wa mzee wa ukoo, Yakobo. Dada yake mdogo, Raheli, ndiye aliyekuwa mke wa pili.—Mwanzo 29:20-29.

 Alifanya nini? Lea alimzalia Yakobo watoto sita. (Ruthu 4:11) Yakobo alikusudia kumwoa Raheli, si Lea. Hata hivyo, baba yao, Labani, akafanya mpango ili Lea achukue nafasi ya Raheli. Yakobo alikasirika alipogundua kwamba ametendewa kwa hila na kupewa Lea, jambo lililokuwa kinyume na makubaliano yao. Lakini alipomuuliza Labani, Labani alimwambia kwamba haikuwa desturi yao kumwoza binti mdogo kabla ya yule wa kwanza. Kisha baada ya juma moja, Yakobo akamwoa Raheli.—Mwanzo 29:26-28.

 Yakobo alimpenda Raheli zaidi ya Lea. (Mwanzo 29:30) Hilo lilimfanya Lea amwonee wivu dada yake, hivyo alikuwa akishindana naye ili aupate moyo wa Yakobo. Mungu aliona hisia zake na akambariki kwa kumpa watoto saba—wana sita na binti mmoja.—Mwanzo 29:31.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Lea? Lea alimtegemea Mungu kupitia sala na hakuruhusu mikazo yake ya kifamilia imkengeushe na kushindwa kuona utegemezo wa Mungu. (Mwanzo 29:32-35; 30:20) Simulizi la maisha yake linaonyesha waziwazi kwamba ndoa ya wake wengi haiwezi kufanikiwa, huo ulikuwa mpango ambao Mungu aliruhusu kwa muda fulani. Kiwango chake cha ndoa ni kwamba mume au mke awe na mwenzi mmoja tu.—Mathayo 19:4-6.

  Martha

 Martha alikuwa nani? Alikuwa dada ya Lazaro na Maria, na wote watatu waliishi karibu na Yerusalemu katika kijiji kinachoitwa Bethania.

 Alifanya nini? Martha alifurahia urafiki wa karibu pamoja na Yesu, ambaye “aliwapenda Martha na dada yake na Lazaro.” (Yohana 11:5) Martha alikuwa mwanamke mkarimu. Wakati fulani Yesu alipowatembelea, Maria alichagua kumsikiliza Yesu huku Martha akiendelea kufanya kazi za nyumbani. Martha alilalamika kwa kuwa Maria hakuwa akimsaidia. Yesu alirekebisha maoni yake kwa fadhili.—Luka 10:38-42.

 Lazaro alipokuwa mgonjwa, Martha na dada yake walimwita Yesu, wakiwa na uhakika kwamba ana uwezo wa kumponya kaka yao. (Yohana 11:3, 21) Lakini Lazaro akafa. Mazungumzo kati ya Martha na Yesu yanaonyesha kwamba alikuwa na imani thabiti kuhusu ahadi ya Biblia ya ufufuo na uwezo wa Yesu wa kumfufua kaka yao ili apate kuishi tena.—Yohana 11:20-27.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Martha? Martha alifanya kazi kwa bidii ili kuonyesha ukarimu. Alikubali shauri alilopewa. Alieleza hisia zake na imani yake waziwazi.

  •  Ili kupata habari zaidi kumhusu Martha, ona makala yenye kichwa, “Nimeamini.”

  Maria (mama ya Yesu)

 Maria alikuwa nani? Alikuwa binti Myahudi, na alimzaa Yesu alipokuwa bikira, hivyo, akamzaa mwana wa Mungu kimuujiza.

 Alifanya nini? Kwa unyenyekevu Maria alifanya mapenzi ya Mungu. Maria alikuwa amechumbiwa na Yosefu wakati alipotokewa na malaika na kujulishwa kwamba atapata mimba na kumzaa Masihi aliyesubiriwa kwa muda mrefu. (Luka 1:26-33) Alikubali jukumu hilo kwa hiari. Baada ya Yesu kuzaliwa, Maria na Yosefu walipata wana wanne na angalau mabinti wawili. Hivyo, Maria hakuendelea kuwa bikira. (Mathayo 13:55, 56) Licha ya kwamba alipewa pendeleo la pekee, hakuwahi kutaka kuabudiwa na hakuwahi kuabudiwa, si wakati wa huduma ya Yesu au wakati alipokuwa mshiriki wa kutaniko la mapema la Kikristo.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Maria? Maria alikuwa mwanamke mwaminifu aliyekubali kwa hiari kupokea jukumu hilo zito. Alikuwa na ujuzi mwingi wa Kimaandiko. Inakadiriwa kwamba alipozungumza maneno yaliyorekodiwa kwenye Luka 1:46-55 alirejelea Maandiko 20 hivi.

  Maria (dada ya Martha na Lazaro)

 Maria alikuwa nani? Alifurahia urafiki wa karibu na Yesu akiwa pamoja na kaka yake, Lazaro, na dada yake, Martha.

 Alifanya nini? Tena na tena alionyesha kwamba alimthamini Yesu kuwa Mwana wa Mungu kwa moyo wake wote. Alikuwa na imani kwamba Yesu angeweza kuzuia kifo cha ndugu yake, Lazaro, na hata alikuwepo Yesu alipomfufua. Dada yake, Martha, alimkaripia Maria alipochagua kumsikiliza Yesu badala ya kumsaidia kufanya kazi za nyumbani. Lakini Yesu alimpongeza Maria kwa kutanguliza mambo ya kiroho.—Luka 10:38-42.

 Wakati fulani, Maria alionyesha ukarimu wa pekee kwa kumpaka Yesu “mafuta ghali yenye marashi” kichwani na miguuni. (Mathayo 26:6, 7) Watu wengine waliokuwepo walimkaripia kwa kuwa walisema kwamba analeta hasara. Lakini Yesu alimtetea kwa kusema: “Popote ambapo hii habari njema [ya Ufalme wa Mungu] itahubiriwa ulimwenguni, jambo alilofanya mwanamke huyu litatajwa pia ili kumkumbuka.”— Mathayo 24:14; 26:8-13.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Maria? Maria alisitawisha imani yenye kina. Alitanguliza ibada ya Mungu badala ya mambo ya kimwili. Kwa unyenyekevu alimwonyesha Yesu heshima, hata ilipomgharimu pesa nyingi kufanya hivyo.

  Maria Magdalene

 Maria Magdalene alikuwa nani? Alikuwa mwanafunzi mwaminifu wa Yesu.

 Alifanya nini? Maria Magdalene alikuwa mmoja wa wanawake kadhaa waliosafiri pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Alitumia pesa zake kwa ukarimu ili kutimiza mahitaji yao. (Luka 8:1-3) Alimfuata Yesu mpaka mwishoni mwa huduma yake, na aliendelea kuwa karibu hata wakati alipouawa. Alikuwa na pendeleo la kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kumwona Yesu alipofufuliwa.—Yohana 20:11-18.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Maria? Maria Magdalene alitegemeza huduma ya Yesu kwa ukarimu na aliendelea kuwa mwanafunzi wake mpaka mwisho.

  Miriamu

 Miriamu alikuwa nani? Alikuwa dada ya Musa na Haruni. Alikuwa mwanamke wa kwanza katika Biblia kuitwa nabii wa kike.

 Alifanya nini? Akiwa nabii wa kike, alikuwa na jukumu la kuwasilisha ujumbe wa Mungu. Alipata cheo kikubwa nchini Israeli na alishirikiana na wanaume kuimba wimbo wa ushindi Mungu alipoharibu jeshi la Wamisri kwenye Bahari Nyekundu.—Kutoka 15:1, 20, 21.

 Baada ya muda fulani, Miriamu na Haruni walikuwa wakimchambua Musa. Ni wazi kwamba waliongozwa na kiburi kikiambatana na wivu wao. Mungu “alikuwa akisikiliza,” na akawakaripia wote wawili vikali, Miriamu pamoja na Haruni. (Hesabu 12:1-9) Mungu akampiga Miriamu kwa ukoma, inaonekana kwa sababu yeye ndiye aliyeanzisha mazungumzo hayo yasiyofaa. Musa alipomsihi Mungu kwa niaba yake, Mungu akamponya. Na baada ya kutengwa kwa siku saba, aliruhusiwa kurudi kwenye kambi ya Waisraeli.—Hesabu 12:10-15.

 Biblia inaonyesha kwamba Miriamu alikubali kurekebishwa. Karne nyingi baadaye, Mungu alirejelea pendeleo la pekee alilompa alipokuwa akiwakumbusha Waisraeli: “Nilimtuma Musa, Haruni, na Miriamu mbele yenu.”—Mika 6:4.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Miriamu? Simulizi la Miriamu lilionyesha kwamba Mungu anasikiliza mambo ambayo waabudu wa Mungu wanazungumzia au mambo wanayosema kuhusu waabudu wenzao. Na pia, tunajifunza kwamba ili kumpendeza Mungu ni lazima tuepuke kuwa na kiburi na wivu—mambo yanayoweza kutufanya tuharibu sifa nzuri za wengine.

  Raheli

 Raheli alikuwa nani? Alikuwa binti ya Labani na mke aliyependwa zaidi na mzee wa ukoo, Yakobo.

 Alifanya nini? Raheli aliolewa na Yakobo na kumzalia wana wawili, ambao walikuja kuwa miongoni mwa waanzilishi wa yale makabila 12 ya Israeli la kale. Raheli alikutana na mwanamume ambaye angekuja kuwa mume wake alipokuwa akichunga kondoo wa baba yake. (Mwanzo 29:9, 10) Alikuwa “mwenye kuvutia sana” akilinganishwa na dada yake, Lea.—Mwanzo 29:17.

 Yakobo alimpenda Raheli, hivyo alikubali kutumikia kwa miaka saba ili ampate. (Mwanzo 29:18) Hata hivyo, Labani alimdanganya Yakobo kwa kumpa Lea kwanza, kisha baadaye akampa Raheli.—Mwanzo 29:25-27.

 Yakobo alimpenda Raheli na watoto wake wawili kuliko alivyompenda Lea na watoto wake. (Mwanzo 37:3; 44:20, 27-29) Jambo hilo lilitokeza ushindani kati ya wanawake hao wawili.—Mwanzo 29:30; 30:1, 15.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Raheli? Raheli alivumilia hali ngumu katika familia bila kupoteza tumaini kwamba Mungu atajibu sala zake. (Mwanzo 30:22-24) Simulizi lake linafunua mkazo unaotokana na ndoa ya wake wengi. Hali aliyopitia Raheli inaonyesha hekima ya Mungu alipoweka kiwango hiki cha ndoa tangu mwanzo—mwanamume awe na mke mmoja tu.—Mathayo 19:4-6.

  Rahabu

 Rahabu alikuwa nani? Alikuwa kahaba aliyeishi kwenye jiji la Wakanaani la Yeriko, na baadaye alikuja kuwa mwabudu wa Yehova Mungu.

 Alifanya nini? Rahabu aliwaficha Waisraeli wawili waliokuwa wakipeleleza nchi. Alifanya hivyo kwa sababu alisikia masimulizi kumhusu Mungu wa Israeli, Yehova, jinsi alivyowakomboa Waisraeli mikononi mwa Wamisri na baadaye alivyowaokoa waliposhambuliwa na kabila la Waamori.

 Rahabu aliwasaidia wapelelezi, kisha akawaomba wasimwangamize yeye na familia yake watakapokuja kuharibu Yeriko. Walikubali lakini walimwekea masharti fulani: Alipaswa kuhakikisha hamwelezi mtu yeyote kuhusu kusudi lao, yeye pamoja na familia yake walipaswa kubaki ndani ya nyumba Waisraeli watakapowashambulia, na alipaswa kuning’iniza kamba nyekundu dirishani ili waweze kutambua nyumba yake. Rahabu alitii kila agizo, hivyo yeye pamoja na familia yake walipona Waisraeli walipovamia Yeriko.

 Baadaye Rahabu aliolewa na Mwisraeli na kuwa nyanya (bibi) ya Mfalme Daudi na Yesu Kristo.—Yoshua 2:1-24; 6:25; Mathayo 1:5, 6, 16.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Rahabu? Biblia inamtaja Rahabu kuwa mfano wa pekee wa imani. (Waebrania 11:30, 31; Yakobo 2:25) Simulizi lake linaonyesha kwamba Mungu ni mwenye kusamehe na hana ubaguzi, akiwabariki wale wanaomwamini, licha ya mambo mabaya waliyofanya zamani.

  Rebeka

 Rebeka alikuwa nani? Alikuwa mke wa Isaka na mzazi wa mapacha wao wawili, Yakobo na Esau.

 Alifanya nini? Rebeka alifanya mapenzi ya Mungu, hata alipokabili hali ngumu akifanya hivyo. Alipokuwa akichota maji kisimani, mwanamume asiyemfahamu alimwomba maji ya kunywa. Rebeka alimpatia maji hayo upesi na tena akajitolea kuchota maji ya kuwanywesha ngamia wa mwanamume huyo. (Mwanzo 24:15-20) Mwanamume huyo alikuwa mtumishi wa Abrahamu, naye alikuwa amesafiri mwendo mrefu ili amtafutie mke Isaka, mwana wa Abrahamu. (Mwanzo 24:2-4) Hata alisali ili apate baraka za Mungu. Alipoona bidii ambayo Rebeka alikuwa nayo pamoja na ukarimu wake, alitambua kwamba Mungu amejibu sala zake, hiyo ndiyo iliyokuwa ishara ya kwamba atamfaa Isaka.—Mwanzo 24:10-14, 21, 27.

 Rebeka alipojua kusudi la safari ya mtumishi huyo, alikubali kuenda naye na kuwa mke wa Isaka. (Mwanzo 24:57-59) Baada ya muda Rebeka akapata mapacha wawili wa kiume. Mungu akamfunulia kwamba yule mwana mkubwa, Esau, angemtumikia yule mdogo, Yakobo. (Mwanzo 25:23) Isaka alipopanga kumpa Esau baraka za mwana mzaliwa wa kwanza, Rebeka alifanya mpango ili kuhakikisha kwamba baraka hizo anapewa Yakobo, kulingana na kile alichojua kuwa mapenzi ya Mungu.—Mwanzo 27:1-17.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Rebeka? Rebeka alikuwa na kiasi, bidii, na alikuwa mkarimu—sifa ambazo zilifanya afanikiwe akiwa mke, mama, na mwabudu wa Mungu wa kweli.

  Ruthu

 Ruthu alikuwa nani? Alikuwa Mmoabu aliyeacha miungu yake na nchi aliyozaliwa ili awe mwabudu wa Yehova katika nchi ya Israeli.

 Alifanya nini? Ruthu alionyesha upendo wa pekee sana kwa mama mkwe wake, Naomi. Naomi, alienda Moabu pamoja na mume wake na wana wao wawili. Walienda huko kwa sababu kulikuwa na upungufu wa chakula nchini Israeli. Hivyo basi wana wao wakaoa wanawake Wamoabu—Ruthu na Orpa. Hata hivyo, baada ya muda, mume wa Naomi na wana wake wawili wakafa na kuacha wanawake hao watatu wakiwa wajane.

 Naomi aliamua kurudi Israeli, ambako ukame ulikuwa umeisha. Ruthu na Orpa walitaka kuenda naye. Lakini Naomi aliwasihi warudi nyumbani kwao. Orpa akakubali kurudi nyumbani. (Ruthu 1:1-6, 15) Kwa upande mwingine, Ruthu, aliamua kushikamana na mamamkwe wake kwa uaminifu. Alimpenda Naomi na alitaka kumwabudu Mungu wa Naomi, Yehova.—Ruthu 1:16, 17; 2:11.

 Ruthu alijitengenezea jina zuri kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwa mama mkwe wake na hata alifanya kazi kwa bidii sana akiwa Bethlehemu, mji wa nyumbani wa Naomi. Boazi, mwanamume tajiri aliyemiliki mashamba alipendezwa sana na mwenendo wa Ruthu, hivyo aliwapatia Ruthu na Naomi chakula kwa ukarimu. (Ruthu 2:5-7, 20) Baadaye Ruthu aliolewa na Boazi, kisha akawa nyanya (bibi) ya Mfalme Daudi na ya Yesu Kristo.—Mathayo 1:5, 6, 16.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Ruthu? Kwa kuwa alimpenda Naomi na alimpenda Yehova, Ruthu aliamua kuacha familia yake na nchi yake kwa hiari. Alifanya kazi kwa bidii, alijitoa kwa uaminifu, hata alipokabiliana na hali nyingi ngumu.

  Sara

 Sara alikuwa nani? Alikuwa mke wa Abrahamu na mama ya Isaka.

 Alifanya nini? Sara aliacha maisha ya starehe kwenye jiji lenye ufanisi la Uru kwa sababu aliamini kwamba ahadi ambazo Mungu alimwahidi mume wake Abrahamu zitatimia. Mungu alimwambia Abrahamu aondoke Uru na kwenda nchi ya Kanaani. Mungu alimwahidi kumbariki na kumfanya kuwa taifa kubwa. (Mwanzo 12:1-5) Kwa wakati huo huenda Sara alikuwa na umri wa miaka zaidi ya 60. Na kuanzia wakati huo, Sara na mume wake walikuwa wakiishi kwenye mahema huku wakihamahama.

 Licha ya kwamba maisha ya kuhamahama yalimhatarisha Sara, aliendelea kumuunga mkono Abrahamu alipokuwa akifuata maagizo ya Mungu. (Mwanzo 12:10, 15) Kwa miaka mingi Sara hakupata mtoto, nalo lilikuwa jambo lililomhuzunisha sana. Lakini Mungu alikuwa amemwahidi Abrahamu kwamba atabariki uzao wake. (Mwanzo 12:7; 13:15; 15:18; 16:1, 2, 15) Kisha, kwa wakati unaofaa, Mungu aliwahakikishia kwamba Sara atamzalia Abrahamu mtoto. Na kwa hakika alijifungua mtoto baada ya kupita umri wa kupata watoto. Alikuwa na umri wa miaka 90, na mume wake alikuwa na umri wa miaka 100. (Mwanzo 17:17; 21:2-5) Walimwita mwana wao Isaka.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Sara? Mfano wa Sara unatufundisha kwamba siku zote tunaweza kumtegemea Mungu kwa sababu tuna uhakika atatimiza ahadi zake, hata tunapoona kwamba ni jambo ambalo haliwezekani! (Waebrania 11:11) Pia, yeye ni mfano mzuri kwa wake, anaonyesha umuhimu wa heshima katika ndoa.—1 Petro 3:5, 6.

  Msichana Mshulami

 Msichana Mshulami alikuwa nani? Alikuwa binti mrembo aliyetoka kijijini na ndiye anayetajwa zaidi katika kitabu cha Wimbo wa Sulemani katika Biblia. Biblia haitaji jina lake.

 Alifanya nini? Mwanamwali Mshulami alibaki mwaminifu kwa mchungaji wake aliyempenda kikweli. (Wimbo wa Sulemani 2:16) Lakini urembo wake wa kipekee ulimvutia sana Mfalme Sulemani aliyekuwa tajiri sana, naye alijaribu kuuteka moyo wake. (Wimbo wa Sulemani 7:6) Licha ya kwamba watu wengine walijaribu kumshinikiza amchague Sulemani, msichana huyo Mshulami alikataa kabisa. Alimpenda kijana mchungaji wa hali ya chini na alikuwa mwaminifu kwake.—Wimbo wa Sulemani 3:5; 7:10; 8:6.

 Tunajifunza nini kutoka kwa msichana Mshulami? Aliendelea kuwa na mtazamo unaofaa kujihusu licha ya urembo wake na jinsi watu walivyopendezwa naye. Hakukubali kushinikizwa na marafiki wala kukengeushwa na ahadi za kupata mali nyingi na umaarufu. Alidhibiti hisia zake na kubaki safi kiadili.

  Mke wa Loti

 Mke wa Loti alikuwa nani? Biblia haitaji jina lake. Lakini inatuambia kwamba alikuwa na watoto wawili na kwamba yeye pamoja na familia yake waliishi ndani ya jiji la Sodoma.—Mwanzo 19:1, 15.

 Alifanya nini? Hakutii amri iliyotoka kwa Mungu. Mungu aliamua kuharibu Sodoma na miji iliyozunguka kwa kuwa walikuwa na mwenendo mchafu sana wa kingono. Kwa kuwa Mungu alimpenda Loti mwadilifu pamoja na familia yake walioishi Sodoma, Mungu akatuma malaika wawili nao wakawasindikiza hadi pahali palipo salama.—Mwanzo 18:20; 19:1, 12, 13.

 Malaika hao waliwaambia watu wa familia ya Loti wakimbie haraka na wasitazame nyuma kwa kuwa watakapotazama nyuma tu, watakufa. (Mwanzo 19:17) Mke wa Loti “akaanza kutazama nyuma, naye akawa nguzo ya chumvi.”—Mwanzo 19:26.

 Tunajifunza nini kutoka kwa Mke wa Loti? Simulizi lake linaonyesha hatari iliyopo ya kupenda vitu vya kimwili na kufikia hatua ya kushindwa kumtii Mungu. Yesu alimtumia kama mfano unaoonya aliposema: “Mkumbukeni mke wa Loti.”—Luka 17:32.

 Mfuatano wa Wanawake Walio Katika Biblia na Wakati Walioishi

  1.  Hawa

  2. Gharika (2370 K.W.K.)

  3.  Sara

  4.  Mke wa Loti

  5.  Rebeka

  6.  Lea

  7.  Raheli

  8. Kutoka (1513 K.W.K.)

  9.  Miriamu

  10.  Rahabu

  11.  Ruthu

  12.  Debora

  13.  Yaeli

  14.  Delila

  15.  Hana

  16. Mfalme wa kwanza wa Israeli (1117 K.W.K.)

  17.  Abigaili

  18.  Msichana Mshulami

  19.  Yezebeli

  20.  Esta

  21.  Maria (mama ya Yesu)

  22. Ubatizo wa Yesu (29 W.K.)

  23.  Martha

  24.  Maria (dada ya Martha na Lazaro)

  25.  Maria Magdalene

  26. Kifo cha Yesu (33 W.K.)