Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 MAHOJIANO | HANS KRISTIAN KOTLAR

Mwanabiolojia Anaeleza Kwa Nini Anamwamini Mungu

Mwanabiolojia Anaeleza Kwa Nini Anamwamini Mungu

Mwaka wa 1978, Dakt. Hans Kristian Kotlar alianza kufanya kazi kwenye Hospitali ya Matibabu ya Kansa nchini Norway, ambapo alifanya utafiti kuhusu kansa na mfumo wa kinga wa mwanadamu. Wakati huohuo alipendezwa pia kujua chanzo cha uhai. Mwandishi wa Amkeni! alimhoji kuhusu utafiti wake na dini yake.

Ni nini kilichokufanya utake kujua chanzo na kusudi la uhai?

Baba yangu alikuwa Mkatoliki na mama yangu alikuwa Mprotestanti. Hata hivyo, hawakuona dini kuwa muhimu. Kwa upande wangu, nilipokuwa tineja, nilitaka kujua kusudi la uhai, nami nilisoma vitabu kuhusu Ubudha, Uhindu, na Uislamu. Hata nilimwomba Mungu anionyeshe ukweli.

Kufikia miaka ya 1970, wanabiolojia wa molekuli walikuwa wamefanya maendeleo yenye kustaajabisha, na nilitaka kujua ikiwa wangefunua chanzo cha uhai. Nilivutiwa na utendaji wa chembe, kwa hiyo niliamua kusomea biolojia. Maprofesa wengi walionifundisha walisema kwamba uhai ulijitokeza wenyewe kupitia utendaji fulani wa kiasili, nami niliwaamini.

Kwa nini ulianza kupendezwa na Biblia?

Mashahidi wawili wa Yehova walitutembelea nyumbani. Ingawa walikuwa wenye urafiki, niliwaambia kwa dharau kwamba sikupendezwa na ujumbe wao. Mke wangu alinisikia. Aliniambia hivi: “Hans Kristian, kwa nini umewatendea kwa dharau hivyo? Si sikuzote umekuwa ukitaka kujua kusudi la uhai?” Nilikubaliana naye. Kwa hiyo niliwafuata haraka Mashahidi hao. Tulipokuwa tukizungumza, niliwauliza ikiwa Biblia inapatana na sayansi.

Walikujibuje?

Walinionyesha yale ambayo Biblia inasema kuhusu Chanzo cha nishati iliyo katika ulimwengu. Walinisomea andiko hili: “Inueni macho yenu juu, mwone. Ni nani ameviumba vitu hivi? . . . Kutokana na wingi wa nguvu zenye msukumo, yeye pia akiwa hodari katika nguvu, hakuna hata moja kati ya hizo inayokosekana.” *  Maneno hayo yalinishangaza. Pia, niliona kwamba Mtu mwenye akili ambaye alitokeza nishati hiyo, ndiye aliyefanyiza ulimwengu wenye utaratibu.

Je, hilo lilibadili maoni yako kuhusu nadharia ya mageuzi?

Hatua kwa hatua, nilianza kugundua kwamba nadharia mbalimbali za mageuzi hazina uthibitisho ulio wazi wa kisayansi. Kwa kweli hizo ni hadithi zilizotungwa ili kueleza jinsi ubuni ulio katika viumbe hai kama vile mfumo wa kinga ulivyojitokeza wenyewe. Kadiri nilivyojifunza kuhusu mfumo wa kinga ndivyo nilivyogundua jinsi ulivyo tata na jinsi unavyofanya kazi kwa utaratibu sana. Kwa hiyo, utafiti wangu ulifanya nifikie mkataa wa kwamba uhai ulitokezwa na Muumba mwenye akili.

Utafiti wangu ulifanya nifikie mkataa wa kwamba uhai ulitokezwa na Muumba mwenye akili

Unaweza kutoa uthibitisho wowote wa kazi ya ubuni?

Kwa kweli mfumo wa kinga umefanyizwa na molekuli, chembe, na mifumo ambayo imekusudiwa kutukinga kutokana na vitu mbalimbali kutia ndani bakteria na virusi. Mifumo hiyo inaweza kupangwa katika vikundi viwili vinavyofanya kazi kwa upatano. Mfumo wa kwanza hushambulia viini saa chache baada ya kuingia mwilini. Mfumo wa pili huchukua siku kadhaa kushambulia lakini hufaulu kushambulia viini hususa kama mshale unaolenga shabaha. Mfumo huo wa pili una kumbukumbu nzuri sana hivi kwamba ikiwa viini ambavyo vilishambulia mwili awali vitarudi miaka kadhaa baadaye, vitaangamizwa mara moja. Mifumo hiyo hutenda kazi kwa njia bora sana hivi kwamba mara nyingi hata hujui kama uliambukizwa, na viini hivyo vikaondolewa. Pia jambo la kustaajabisha ni kwamba mfumo wa kinga unaweza kutofautisha kati ya viini vinavyoingia mwilini na mamia ya chembe mbalimbali ambazo hufanyiza mwili wetu.

Tueleze, ni nini hutendeka viini vinapoingia mwilini?

Viini huingia mwilini kupitia hewa tunayopumua, chakula, viungo vya uzazi na mfumo wa mkojo, au jeraha kwenye ngozi. Mfumo wa kinga unapogundua kwamba viini vimeingia, unaanza mfululizo wa utendaji unaohusisha protini nyingi zilizopangwa kihususa. Kila utendaji katika mfululizo huo huanzisha ule unaofuata ili kuimarisha mashambulizi. Utendaji huo unastaajabisha sana!

Kwa hiyo, je, ujuzi wako wa sayansi umeimarisha imani yako katika Mungu?

Bila shaka! Uwezo na utata wa mfumo wetu wa kinga unaonyesha kwamba kuna Muumba mwenye hekima na upendo. Naweza kusema pia kwamba sayansi imeimarisha imani yangu katika Biblia. Kwa mfano, Methali 17:22 inatuambia kwamba “moyo wenye shangwe ni dawa nzuri.” Watafiti wamegundua kwamba hali yetu ya akili inaweza kuathiri mfumo wetu wa kinga. Kwa mfano, mkazo unaweza kudhoofisha mfumo wetu wa kinga.

Wanasayansi wengi hawaamini kuna Mungu. Kwa nini?

Kuna sababu nyingi. Wengine wao wanakubali tu kile walichofundishwa. Huenda wanaamini kwamba nadharia ya mageuzi inaungwa mkono na mambo hakika ya kisayansi. Wengine hawajishughulishi kujua chanzo cha uhai. Jambo hilo linasikitisha. Kwa maoni yangu, wanapaswa kuuliza maswali zaidi.

Kwa nini uliamua kuwa Shahidi wa Yehova?

Nilivutiwa na ukarimu wao na yale wanayoamini kuhusu ahadi ya Muumba ya wakati bora ujao. * Yale wanayoamini yanategemea utafiti na mambo hakika, na si hadithi au mambo ya kukisia-kisia tu. *